Atletico yachelewesha sherehe za Barcelona za ubingwa wa ligi

Atletico Madrid walichelewesha Barcelona kubeba ubingwa wa La Liga kwa siku chache angalau baada ya Alvaro Morata na Antoine Griezmann kufunga bao moja kila mmoja katika ushindi wa 3 – 2 dhidi ya Valencia Jumatano. Bao la tatu lilifungwa na Angel Correa katika dakika ya 80

Kichapo katika dimba la Wanda Metropolitano kingewavisha Barca taji la mafalme wa kandanda Uhispania kwa mara ya 26 katika historia yao, ambapo sasa vijana hao wa Catalans watasherehekea katika uwanja wao wenyewe wa Camp Nou Jumamosi ijayo.

Barca wakipata ushindi dhidi ya Levante basi watakuwa mabingwa wa Uhispania, taji lao la nne la ligi katika miaka mitano na wataweza hata kufanya hivyo kama Atletico watashindwa kuchukua pointi moja nyumbani dhidi ya Real Valladolid mapema siku hiyo.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments