Bayern mkono mmoja kwenye taji, Dortmund wateleza

Vinara wa Bundesliga Bayern Munich walipata ushindi wa 3 – 1 dhidi ya washika mkia Hannover Jumamosi na sasa wanahitaji kushinda mechi moja tu na kunyakua taji lao la saba mfululizo la Bundesliga.

Ushindi huo umetanua uongozi wao kileleni na pengo la pointi nne dhidi ya Borussia Dortmund, ambao waliongoza 2 – 0 dhidi ya Werder Bremen huku zikiwa zimesalia dakika 20 mechi kukamilika lakini wakafungwa mabao mawili na kutoka sare ya 2 -2, wakati timu zote mbili zikiwa na mechi mbili zilizobaki kuchezwa msimu huu.

Robert Lewandowski na Leon Goretzka waliwaweka Bayern 2-0 kifua mbele katika kipindi cha kwanza lakini mambo yakageua baada ya Jonathas kufunga bao moja kupitia penalty yenye utata iliyotolewa baada ya Jérôme Boateng, kuunawa mpira katika dakika ya  51. Jonathas kisha alitimuliwa uwanjani baada ya kushikana mashati na Joshua Kimmich katika dakika ya 55.

Bayern hatimaye wakahitimisha kichapo hicho baada ya Franck Ribéry kuingia uwanjani kama nguvu mpya na kuwapa bao la tatu kunako dakika ya 84.

Dortmund walikabiliwa na mechi ngumu ugenini dhidi ya Bremen na Christian Pulisic akafunga bao la mapema katika dakika ya sita ili kutuliza mambo.

Paco Alcácer aliongeza la pili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika lakini mabao mawili ya kipindi cha pili kutoka kwa Kevin Mohwald na Claudio Pizarro yakaipa Bremen sare na kuiweka Bayern katika nafasi nzuri katika mbio za kuwania ubingwa

Author: Bruce Amani

Facebook Comments