Biashara yafanya biashara mapema na Yanga

Yanga imepoteza mchezo wa pili mfululizo tangu uongozi mpya uingie madarakani huku Mwinyi Zahera akionekana kama haelewi kinachoendelea klabuni hapo na wachezaji wakiwa hawajitumi vya kutosha.

Katika mchezo uliochezwa uwanja wa Karume Msoma, Mara Yanga imeangukia pua kwa goli 1-0 na kuendelea kufifisha matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara kwani sasa inahitaji zaidi maajabu kuliko mahesabu.

Goli pekee lililoamua mchezo huo limewekwa kimiani na mshambuliaji Tariq Seif katika dakika ya 8 tu ya mchezo baada ya mabeki wa Yanga kumuacha mchezaji huyo peke yake wakidhani ameotea huku likiwa ni shambulizi la kushitua.

Pamoja na mabadiliko ya kocha Mwinyi Zahera hayakuisaidia timu hiyo kupata matokeo ya alama tatu.

Matokeo hayo yanaifanya klabu ya Biashara kufikisha alama 40 kutoka 37 ambazo walikuwa nazo kabla ya mechi ya leo sawa na 18.

Yanga nao wanazidi kusalia na alama zao 80 wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na wakiwa wamecheza jumla ya mechi 35, wakizidiwa na mpinzani wake Simba mwenye pointi 81.

Uchaguzi wa Yanga umeingia na mkosi ndani ya timu hiyo kwani tangu kuingia madarakani timu haijapata matokeo katika mechi zote mbili, ile FA dhidi ya Lipuli na Biashara leo.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments