Bocco arejea kikosini Simba, Wawa bado mkekani

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Simba SC inaingia uwanjani Jumatano Mei 8, kucheza dhidi ya Wagosi wa Kaya Coastal Union katika mtanange wa Ligi Kuu ya Kandanda Tanzania Bara mchezo utakaofanyika dimba la Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba wanaingia kwenye mchezo huo ikiwakosa wachezaji wao muhimu kutokana na majeruhi yanayowakabili wachezaji wa timu hiyo.

Pascal Sergio Wawa, Shomary Kapombe, na Asante Kwasi wataukosa mtanange wa leo huku kukiwa na taarifa ya kurejea kwa Nahodha wa kikosi cha timu hiyo John Raphael Bocco.

Akizungumzia maendeleo ya wachezaji wa timu hiyo kuelekea mchezo wa leo, Meneja wa klabu ya Simba Patrick Ruyemamu amesema watakosekanika wachezaji watatu ambao hata mechi zilizopita hawakuwa sehemu yetu.

“Mechi ya leo tunawakosa wachezaji watatu, tutamkosa Pascal Wawa ambaye bado hajaanza kufanya mazoezi, tutamkosa pia Asante Kwasi na Shomary Kapombe ambao wameanza kufanya mazoezi ya kibinafsi. Alisema Patrick ambaye ameteuliwa kuchukua mikoba ya Mussa Hassan Mgosi.

Kapombe alipata majeruhi akiitumikia timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars wakati ikijiandaa na mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Lesotho, tangu hapo amekuwa mchezaji wa machera bila kucheza mchezo hata mmoja kwa upande wa Simba.

“John Raphael Bocco amerejea kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza, kuhusu kutumika kwenye mchezo wa leo ni maamuzi ya Mwalim kumtumia lakini kikubwa ameanza kufanya mazoezi” Aliongeza Patrick Ruyemamu.

Bocco hakuwa sehemu ya kikosi cha Simba katika michezo miwili iliyofanyika jijini Mbeya ambapo yote Simba ilishinda dhidi ya Mbeya city na Tanzania Prisons.

Simba inahitaji ushindi dhidi ya Coastal Union kuendelea kuipa shinikizo klabu ya Yanga ambayo ni kinara kwenye msimamo wa Ligi kuu bara.

Ratiba ya TPL Mei 8.
Mtibwa Sugar 10:00 JKT Tanzania
Uwanja: Turiani, Morogoro.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments