Heiko ataiokoa Leverkusen?

Ligi ya Ujerumani imo katika kipindi cha mabadiliko katika sekta ya makocha. Makocha wengi wanaovutia viongozi wa vilabu ni vijana wadogo wenye uwezo mkubwa wa kutumia kompyuta na wenye mbinu nyingi. Unapozungumzia hilo unawazungumzia makocha kama Domenico Tadesco wa Schalke 04 ama Julian Nagelsmann wa TSG Hoffenheim.
Na kutokana na mtazamo huo vilabu vingi vya Bundesliga vinaweza kuyumba mara timu zao zinapokutwa na majanga ya kuuanza vibaya msimu. Moja ya timu ambazo zinaelekea kuyumba ni Bayer 04 Leverkusen. Timu hii inayoongozwa na kocha Heiko Herrlich imepoteza michezo yote miwili ya mwanzo. Imefungwa na Wolfsburg nyumbani 1-3 na mchezo wa kwanza ilifungwa  na Borussia Moenchngladbach 2-0. Mbaya zaidi baada ya mapumzuko kupisha michezo ya timu ya taifa Die Mannschaft, Bayer Leverkusen inapambana katika mchezo wa tatu wa Bundesliga na mabingwa watetezi Bayern Munich na baada ya mchezo wa ligi ya Ulaya itapambana na Mainz 05.
Hii ni changamoto kubwa kwa kocha Heiko Herrlich ambaye aliwahi kuichezea timu hiyo pamoja na kupata mafanikio makubwa pamoja na ubingwa wa Champions league  akiwa na Borussia Dortmund. Je iwapo atashindwa dhidi ya Bayern na kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo ya Ulaya, Herrlich kiti chake kitayumba?
Mwenyewe ana imani kwamba ataweza kubadili mwelekeo wa timu yake. Hata mkurugenzi wa spoti wa Leverkusen Jonas Boldt anakanusha minong’ono ya viongozi kusaka kocha mwingine. Lakini meneja wa zamani wa  Leverkusen Reiner Calmund anasema kiongozi wa Leverkusen Rudi Voller ni mchezaji aliyefikia kuwa mchezaji wa timu ya taifa na kocha pia , akijisikia kuwa mambo hayendi atachukua hatua haraka kuiokoa Leverkusen kutumbukia katika janga.
Minong’ono imetanda hata hivyo kwamba viongozi wanawatupia jicho makocha kadhaa, licha ya kuwa si vijana hiivyo. Mmojawapo ni Ralph Hasenhuetl aliyekuwa akiifunza RB Leipzig , Markus  Weinzierl aliyeitumikia Augsburg na kisha Schalke 04 kwa msimu mmoja tu. Pia kuna jina la Markus Gisdol aliyewahi kuwa kocha wa TSG Hoffenheim na kisha Hamburger SV.
Herrlich lakini anakumbana na tatizo la kupungukiwa wachezaji wake hasa wa ulinzi mapacha Lars Bender na Sven Bender. Ukuta wa Leverkusen unayumba kwa kukosekana wachezaji hawa ambao ni majeruhi. Watakaporejea na kuwa fit wataleta uzoefu mkubwa walionao katika kikosi cha kocha Heiko Herrlich na huenda wakamuokoa kibarua kisiote majani.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments