Kenya yaikaba Ethiopia na kuongoza Kundi F

Harambee Stars imechukua usukani wa Kundi F katika michuano ya kufuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika – AFCON 2019 baada ya kuwakaba wenyeji Ethiopia kwa sare tasa katika uwanja wa Bahir Dar mjini Addis Ababa Jumatano jioni.

Vijana wa Kenya walistahimili mashambulizi ya kipindi cha pili kutoka kwa timu ya nyumbani iliyoaidiwa na mashabiki waliofurika uwanjani.

Sare hiyo ina maana kuwa Stars wanapanda kileleni mwa Kundi F na pointi nne baada ya kuwazaba Ghana na sasa kama watashinda mechi ya marudiano dhidi ya Ethiopia katika uwanja wa Moi Kasarani Niarobi Jumapili ijayo watakaribia kufuzu katika dimba la AFCON kwa mara ya kwanza 2004.

Shirikisho la Kandanda Afrika CAF halijafanya maamuzi ya kama matokeo ambayo timu nyingine zilipata kutokana na mechi dhidi ya Sierra Leone – ambao wanachunguzwa na FIFA – yatahesabiwa katika safari ya kufuzu.

Mchuano wa Sierra Leone uliotarajiwa kuchezwa leo dhidi ya Ghana ulifutwa baada ya Sierra Leone kushindwa kuwarejesha katika nyadhifa zao maafisa wa shirikisho la kandanda la nchi hiyo waliotimuliwa.

Author: Bruce Amani

Facebook Comments