Kila la heri Kenya, Tanzania na Uganda

Wiki hii timu za Taifa za Tanzania Taifa Stars, Kenya Harambee Stars na Uganda The Cranes, kwa nyakati tofauti zitashuka dimbani kurusha karata kujaribu kutafuta nafasi za kufuzu kwa michuano ya Mataifa ya Afrika Afcon inayotarajiwa kurindima 2019 nchini Cameroon.

Harembee Stars wao watakua wa kwanza kurusha karata yao hapo kesho Oktoba 10 Nchini Ethiopia katika mchezo muhimu wa kundi F unaotarajiwa kuvurumishwa katika Jiji la Adis Ababa.

Huu ni mchezo muhimu sana kwa vijana wa Harambee Stars ambao kimahesabu wanahitaji pointi nne tu ili waweze kufuzu kwa michuano hii hapo mwakani

Ikumbukwe kwamba Harambee Stars inasaka nafasi ya kufuzu ikiwa na kumbu kumbu ya miaka takribani kumi na nne kutoonekana katika fainali hizi na mara ya mwisho ilikua mwaka 2014 kule Tunisia chini ya Kocha Mzalendo Jacob ’Ghost’ Mulee.

Kuondolewa kwa Sierra Leone katika michezo ya Kimataifa na FIFA inafanya kundi F kusalia na timu tatu ambazo ni Kenya, Ghana na Ethiopia hivyo kundi hili linahitaji mahesebu ili kupata nafasi ya kufuzu.

Kenya ilianza kampeni ugenini dhidi ya Sierra Leone kwa kupoteza kwa magoli 2 – 1 lakini wakaja kuwaduwaza Ghana kwa kuwadonyoa goli 1 – 0, huku Ghana wakiwafunga Ethiopia magoli 5 – 0 na kwa upande wa Ethiopia wakiwafunga Sierra Leone magoli 2 – 1 ambao wameondolewa katika michuano ya kimataifa kutokana na kile kinachosemekana na serikali ya nchi hiyo kuingilia katika masuala ya kimichezo, na matokeo yake yote kufutwa hivyo kuinufaisha Kenya ambayo ilipoteza mchezo dhidi ya Sierra Leone

Katika kundi F, Ghana na kenya wote wana pointi 3 huku Ethiopia inasalia bila ya pointi na endapo Kenya itapata matokeo katika mchezo wao wa ugenini dhidi ya Ethiopia basi itajiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kwani itahitaji pointi moja zaidi katika michezo miwili iliyosalia. Mmoja watacheza nyumbani dhidi ya Ethiopia na ule wa ugenini dhidi ya Ghana

Kimahesabu Kenya inaweza kuibuka na ushindi ugenini sababu kubwa katika mchezo uliopita waliwafunga Ghana moja ya timu bora barani Afrika ukifananisha na timu ya Ethiopia ingawa mpira hauamuliwi kwa njia hivyo, na kila mchezo una mtazamo wake, kama jitihada zitafanyika basi hapa ndipo pa Kenya kuchukua matokeo bora na kuibukia kule Cameroon 2019.

Tahadhari yangu kwa Harambee stars:

Timu ya Taifa ya Ethiopia mara nyingi huwa haipewi nafasi ya kufanya vema katika michuano ya Kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na kile kinachoonekana haina kikosi bora au wachezaji wanaotamba barani Afrika na kwingineko, hata katika ubora wa viwango vya FIFA ipo katika nafasi ya 149 ukifananisha na Kenya iliyosalia katika nafasi ya 107, lakini mpira umebadilika sana katika miaka ya karibuni na timu yeyote inaweza kupata matokeo dhidi ya timu bora

Ethiopia imekua timu ngumu kudondosha pointi tatu hasa ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani na katika michezo mitano ya mwisho ya timu hiyo ikiwa nyumbani imechomoza na ushindi katika michezo mitatu dhidi ya Lesotho, Seychelles na Sierra Leone na kutoka sare michezo miwili dhidi ya Mali na Algeria mara ya mwisho kufungwa nyumbani ilikua miaka minne iliyopita mwaka 2014 na Algeria katika uwanja wake wa nyumbani

Hivyo Kenya inahitaji kuchukua tahadhari ya hali ya juu katika mchezo huo ili wapate matokeo bora na kujiweka katika mazingira mazuri katika kundi F, na kama watashinda watakuwa vinara wa kundi hili kwa kufikisha pointi sita huku wakisalia na michezo miwili, na kama unafahamu washindi wawili wa kwanza wa kila kundi wanafuzu katika michuano ya afcon 2019 .

Ijumaa ya wiki hii siku ya tare 12 Oktoba, 2018 katika Mji wa Praia nichini Cape Verde timu ya Taifa ya Tanzania nayo itajaribu bahati yake ugenini dhidi ya timu ngumu ya Cape Verde.

Tanzania ipo kundi L sambamba na Uganda, Lesotho na Cape Verde, Uganda Wanaongoza kundi hili kwa kujikusanyia alama 4 kwa michezo miwili Tanzania na Lesotho wakiwa na alama mbili katika nafasi ya pili na ya tatu, huku Cape Verde akiburuza mkia kwa kuwa na alama moja

Kama Taifa Stars itapata matokeo chanya dhidi ya wenyeji wao Cape Verde basi itajiweka katika mazingira bora ya kufuzu kwa mara ya kwanza baada ya timu hiyo kufuzu katika fainali za AFCON mwaka 1980 kule Lagos Nigeria

Stars ikiongozwa na kocha Emanuel Amunike raia wa Nigeria bado haijapata alama tatu kwa pamoja katika michezo ya awali lakini pia haijadondosha alama zote tatu katika michezo hiyo miwili ya awali

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kwenda Mjini Praia kupambana na Cape Verde mara ya kwanza ilikua mwaka 2008 chini ya kocha Mbrazil Marcio Maximo Stars ilitota kwa kulala kwa goli 1 – 0 kabla ya kulipiza kisasi jijini Dar-Es Salaam kwa kuwavuruga kwa magoli 3 – 1

Taifa Stars kwa sasa inaonekana imeaanza kuimarika na kuwa na kikosi bora kutokana na baadhi ya wachezaji kutoka nje ya Tanzania kusakata kandanda, kama watachanga vema karata zao basi huenda wakatoa mkosi wa kutoshiriki katika fainali za michuano mikubwa kama hii,

Uganda The Creams moja ya timu bora katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati na ni timu ya mwisho toka ukanda wetu kushiriki katika fainali za Afcon ikifanya hivyo mwaka 2017 kule Gabon, inaonekana ipo katika nafasi nzuri ya kufuzu kwa mara nyingine tena kutokana na kuanza vema katika michezo ya kundi L

Siku ya Jumamosi ya 13 Oktoba 2018 watakua pale Nambole dhidi ya Lesotho na kama itapata ushindi basi itaiamarisha nafasi yake ya uongozi wa kundi na pia kujiweka vema kuelekea Cameroon 2019

Nikiwa mwana Africa Mashariki nazitakia matokeo bora timu zote tatu ili pengine tuandikishe rekodi kwa mara ya kwanza timu tatu za ukanda wa Afrika Mashariki kwa pamoja kufuzu kwa michuano ya AFCON

Author: Bruce Amani

Facebook Comments