Nini cha kuvuna kutokana na ujio wa Sevilla nchini Tanzania?

Shirikisho la soka nchini, TFF, limetangaza ada za kiingilio kwa mchezo wa kimataifa utakaowakutanisha mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC na Sevilla FC kutoka nchini Hispania. Tiketi za VIP zitakuwa shilingi 5,000, VIP B 15,000 na Platinum 100,000

Wahenga husema “Mgeni njoo mwenyeji apone” kauli hii ikitumiwa vyema katika ujio wa Sevilla basi pasi na shaka matunda mema yatazaliwa katika urafiki wa mechi hii.

Sevilla ni miongoni mwa timu zilizofanikiwa barani Ulaya ikiwa imetwaa ubingwa wa Europa League mara tano, jambo ambalo si la kubezwa hata kidogo badala yake ni sayansi katika kufikia hapo.

Mafanikio yake yanaweza kuhamia kwetu (Simba). Hii inawezekana hasa katika kipindi hiki ambacho Simba ipo katika hali nzuri ya kiuchumi, kila jambo lawezekana.

Ujio wao utawaleta viongozi wa ufundi ambao wanaweza kuongea na Viongozi wa hapa nyumbani na kubadilishana namna Sevilla wanavyoendesha masuala ya soka klabuni kwao. Sio jambo baya kujifunza kwa aliyetangulia.

Pili, Unaweza ukaleta mwanzo wa ushirikiano baina ya timu hizi mbili kwenye uzalishaji wa vijana. Kwa mfano Simba inaweza ikaomba kila msimu iwe inapeleka vijana wa idara tatu katika vituo vya kukuzia watoto vya Sevilla, jambo litakalosaidia kuinua mpira wa nchi.

Tatu, ujio wao utoe elimu namna ambavyo viongozi wao wanaendesha mambo kiuweledi kuliko sisi. Wapi wamefanikiwa wapi tunashidwa. Hii itasaidia hata wakiondoka ujuzi wao kubakia.

Ni siku chache watakaa hapa nchini ila zinatosha kupata yale muhimu kuliko kuishia kuongea mambo yasiyo na manufaa na mkamalizia kupiga picha ufukweni.

Shime hata viongozi wa Yanga mnaweza kwenda kupata uzoefu huo. Maendeleo sio chama au kabila popote pale unapata.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments