Simba yaanza kutafuna viporo vyake katika ligi kuu

Takribani siku 40 mabingwa watetezi wa taji la ligi kuu Tanzania Wekundu wa Msimbazi Simba walikosekana katika patashika ya ligi kuu, Leo hii Alhamisi imeshuka dimbani ma kuchomoza na ushindi mujarabu wa magoli 3-0 dhidi ya wachimba madini ya almasi toka mkoani Shinyanga Mwadui FC

Ilichukua dakika 45 tu za kipindi cha kwanza kwa Wekundu hao wa Msimbazi toka Kariakoo kujihakikishia pointi zote tatu baada ya kufunga magoli hayo kupitia kwa mshambuliaji wake mwenye uchu wa magoli Meddie Kagere, kiungo Muzamil Yassin aliipatia goli la pili kunako dakika ya 25 kabla ya nahodha wa mabingwa hao watetezi John Rafael Boko kutupia goli la 3 na kuhitimisha karamu hiyo ya magoli

Kwa ushindi huo Simba imerejea katika nafasi ya tatu ya msimamo na kujikusanyia alama 36 sawa na Lipuli FC wakitofautiana kwa wastani wa magoli ya kufunga na kufungwa lakini Simba akicheza michezo 15 Lipuli akishuka dimbani mara 24

Mabingwa wa kihistoria wa ligi ligi hiyo Young Africans licha ya kusuasua katika ligi kwa michezo mitatu mfululizo bado wanaongoza katika jeduwali la msimamo wakiwa na alama 55 baada ya michezo 22 huku Azam akishika nafasi ya pili kwa kujikusanyia alama 48 baada ya michezo 21

Ligi hiyo itaendelea tena wikiendi hii kwa Yanga kuwavaa maafande wa JKT Tanzania katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku waoka mikate wa Azam FC wakiwa katika dimba la Zamora Iringa kuwavaa wana paluhengo Lipuli FC

Author: Master Tindwa

Facebook Comments