Simba yawapigisha kwata maafande wa Magereza

Simba SC imevuna alama zote tatu katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine Jijini Mbeya baada ya kuifunga klabu ya Tanzania Prisons kwa goli 1-0 ukiwa ni muendelezo wa ratiba maalumu iliyonayo klabu ya Simba kukamilisha viporo vya Ligi Kuu Tanzania bara.

Simba siku ya Ijumaa iliifunga Mbeya City goli 2-1 hapo hapo Sokoine wakiwa wametokea nyuma kwa goli lilofungwa na Iddi Nado.

Katika mchezo wa leo Simba ilipata goli pekee kupitia kwa Emmanuel Okwi baada ya kutegeana kwa mabeki na mlinda mlango wa Tanzania Prisons Aroni Karambo kwa mpira mrefu uliokuwa umepigwa kutokea nyuma.

Goli hilo liliifanya Simba kujiamini baada ya kuanza kuonyesha kiwango bora huku Haruna Niyonzima na Clatous Chama wakiongoza sehemu ya kiungo kutandaza kandanda safi.

Kipindi cha pili kilianza kwa Maafande wa Magereza, Tanzania Prisons kumuingiza Sabianka katika kuongeza nguvu ushambuliaji jambo lililowasaidia kutawala mchezo kwa muda mrefu.

Akizungumza baada ya mchezo huo Nahodha msaidizi Erasto Nyoni amesema waliingia kipindi cha kwanza kupata matokeo lakini kipindi cha pili kocha (Patrick Aussems) aliwaambia wajikinge kwa sababu walikuwa wamepata matokeo tayari.

Upande wa Nahodha wa Wajela Jela Tanzania Prisons amesema kushindwa kutumia nafasi chache zilizopatikana zimepelekea kupoteza mchezo huo, kwani wapinzani wetu wametumia nafasi moja iliyopatikana.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha alama 78 katika nafasi ya pili ikiwa imecheza michezo 30 na kubakiwa na mechi nane tu msimu 2018/2019 kumalizika.

Wakati ambao Tanzania Prisons wamesalia na alama zao 42 kwenye michezo 33 ambayo imecheza mpaka sasa katika Ligi Kuu Tanzania bara.

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments