Yanga kuivaa Biashara bila ya huduma za nahodha Ajib

Mabingwa wa Kihistoria wa ligi Kuu ya kandanda Tanzania bara, Kikosi cha Yanga Ijumaa kinashuka dimbani kumenyana na Biashara FC ya Mara, katika mtanange utakaofanyika uwanja wa Karume mjini Musoma.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo bila ya huduma ya Nahodha wao mkuu Ibrahim Ajib ambaye amerudishwa Dar es Salaam mara baada ya kupata changamoto ya kiafya, uongozi wa klabu hiyo umeeleza kupitia vyanzo mbalimbali vya habari.

Wanajangwani Yanga wanaingia kwenye mchezo dhidi ya Biashara wakiwa wameshushwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi na alama 80 dhidi ya 81 za Simba. Yanga itahitaji ushindi wa aina yoyote ili kukwea juu ya Simba ambayo ni kinara wa ligi kwa alama moja zaidi ya Yanga huku Simba akinufaiki na idadi ya mechi alizocheza.

Yanga itaweza kurejea kileleni endapo itashinda mchezo wa kesho na Simba iende sare ama ipoteze dhidi ya Kagera Sugar. Biashara United wamekuwa na historia nzuri ya kuitaabisha Yanga kupata matokeo kiurahisi kumbuka hata mechi ya FA, Yanga ilihitaji dakika za lala salama kuokoa na aibu ya kufungwa uwanja wa Taifa. Tangu achukue timu Amri Said timu imebadilika kiuchezaji kabisa.

Wakati huo huo Klabu ya Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti Mwakalebela imepokea kitita cha shilingi milioni 20 kutoka kwa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Yiovele kama sehemu ya mchango wake kwa klabu.

Matokeo mechi za Mei 9

*Azam 0 – 0 KMC
*Alliance 3 – 1 Mwadui Fc
*African Lyon 2 – 3 Mbao
* Ruvu Shooting 2 – 0 Lipuli
* Stand United 2 – 2 Singida UnitedY

Author: Asifiwe Mbembela

Facebook Comments